Wednesday, June 22, 2016


Safari inapoanzia

Ni matumaini yangu kwamba tupo pamoja. Kila kunapokucha tunakutana na mambo mengi, mambo yote hayo tunayokutana nayo yana lengo moja tu kutujenga au kutuharibu. Safari inaanza pale mtu anapozaliwa. Nasema safari inaanzia hapo kwa sababu ya kitu ninachotaka kujadili na wewe kwenye makala hii. Hakuna mtu aliyezaliwa kwa kuchagua azaliwe na nani na wapi bali kila mtu amejikuta amezaliwa hapo alipo. Mara baada ya kuzaliwa safari ya maisha inaanza na hapo ndipo kila mtu hukua kwa aina yake sawa sawa na malezi atakayofundishwa. Kutokana na utofauti huu wa maisha na mahali unapoishi, Serikali nyingi duniani zikaandaa utaratibu wa kufuata kwa watu wote wanaokua. Utaratibu huu unaitwa Elimu ya Taaluma na ili kuhakikisha kila mtu anakua kwa misingi ya taifa lake, serikali ikaandaa silabasi ambazo kila mtu atafundishwa kupitia silabasi hizo. Hapo ndipo safari ya maisha ya mtu inapoendelea kusonga mbele. Mimi na wewe tu mashahidi wa silabasi hizo.

Kuanzishwa Kwa Shule Mwanzo Wa Fikira Mpya Na Matatizo Mapya
Siandiki makala hii kupingana na utaratibu wa kuwepo kwa shule. Shule ni msaada mkubwa sana kwa kila mtu. Kwa sababu kupitia shule tunaweza kufunguka akili zetu na kujifunza mambo mengi ambayo bila kupitia shule siyo rahisi kuyafahamu yote. Kusoma shule ni mwanzo wa kuibua fikira mpya akilini mwetu na kuongeza upeo wa kufikiri zaidi na kuongeza upeo wa kukabiliana na changamoto zinazotukabili.
Hata hivyo kuwepo kwa shule kumeibua tatizo kubwa miongoni wa jamii. Mwaka 2014 nilikutana na vijana waliohitimu kidato cha nne katika shule moja ya kata iko wilaya ya Nzega. Matokeo yao ya kuhitimu kidato cha nne hayakuwa mazuri kabisa au niseme walifeli.
Siku hiyo nilikutana nao Nzega mjini wakaanza kuniambia mambo mengi lakini katika mambo yote waliyosema yalikuwa na dalili ya kukata tamaa. Walikuwa ni wawili na wote walikuwa wamekata tamaa kabisa hawakuwa na matumaini hata kidogo mioyoni mwao.

Jinsi Nilivyowajibu Hoja Zao
Mara walipomaliza kunieleza na kunionyesha kwamba hawakuwa na matumaini niliwaambia jambo moja, nilisema hivi “Nyanyueni shingo zenu angalieni pande zote hapo mlipo kisha niambieni mmeona nini?” Haikuchukua dakika tano wakaniambia tumeona nyumba na magari na watu na miti. Nikawaambia tena. “ Nendeni kwenye nyumba hizo na kwenye magari hayo ulizeni kila mmiliki wa nyumba na gari mtakayemkuta muulizeni amesoma mpaka digirii ngapi ndipo akajenga nyumba hiyo au akanunua gari yake? Watakavyo waambia njoni mniambie.

Walitafakari sana baada ya muda wakasema kwanini kaka unatuambia hivyo?. Nikawaambia wamiliki wa majumba hayo makubwa mnayoyaona na wamiliki wa magari mazuri hayo mnayoyaona wengi wao waliishia darasa la saba. Wachache walimaliza kidato cha nne na wachache zaidi waliosoma elimu ya chuo.
Nikaendelea kuwaambia, nyinyi mnaniambia maneno hayo yote na tena mmekata tamaa kwasababu mnapingana na kile Mungu alichokiweka ndani yenu. Mungu aliamuru akili zenu zikae kichwani mwenu lakini leo hii nyinyi mnang’ang’na na kutamani akili zenu mziweke kwenye kipande cha karatasi kinachoitwa cheti. Hiyo pekee ndiyo inayowafanya muwe na huzuni na kukata tamaa. Na huzuni hiyo haitaondoka mpaka mtakapo kubali akili zenu zikae kichwani mwenu ndipo huzuni hiyo itatoka. Awali Hawakunielewa nilichokuwa naongea lakini baadaye walinielewa walishukuru sana walitoka na nguvu mpya.

Vurugu Ilipoanzia Na Itaendelea Kukuchanganya
Natamani sana niwe na utaratibu wangu wa maisha tofauti kabisa na uliopo. Lakini siwezi kufanya hivyo kwa sababu kila mtu anajua kwamba ni lazima usome na ukimaliza masomo yako upewe cheti kuonyesha kwamba umesoma. Kinachoniudhi mimi sio kusoma bali ni hicho cheti. Sio kwa sababu kupewa cheti ni vibaya bali cheti kinaficha akili nyingi za watu. Hata mimi vyeti vyangu vimeficha akili zangu kwa muda mrefu,  taratibu ndipo nimeanza kuligundua hili. Hebu nikupe kilelezo cha kweli.

Mfano halisi: Wakati nasoma chuo nimesoma na watu wenye umri tofauti tofauti, kulikuwa na vijana pia kulikuwa na watu wazima. Katika hao wote nilichokuwa nawasikia wanasema ni kwamba wanasoma ili wapate cheti. Ilikuwa ni jambo la kusikitisha pale mwenzetu anapofukuzwa chuo kwa kushindwa kufikia kiwango cha ufaulu kilichowekwa. Tulikuwa hatusikitiki kwa sababu mwenzetu tutammiss bali tulikuwa tunasikitika kwa sababu amekosa cheti.
Nimekutana na watu mbalimali maofisini wenye elimu tofauti tofauti wapo wenye astashahada, stashahada, shahada, masters na PHD. Kilichonishangaza nikwamba sijaona matokeo ya wazi ya watu hawa yaliyoletwa kutokana na utofauti wa elimu zao. Au kwa maneno mengine ni kwamba nilitegemea wenye elimu kubwa waonyeshe ujuzi wao au wafanye mambo yanayoonekana kwa jamii kutokana na elimu zao. Nilichokiona ni utofauti wa vyeo tu.

Nilijaribu kuwahoji baadhi yao kuhusiana na hili,  nilichoambulia kuambiwa ni hiki “ Kama unafikiri nakudanganya ngoja nikuletee cheti changu cha masters”. Nilisikitika sana ndipo nikagundua kumbe watu wengi wanasoma kisha akili zao wanaziacha kwenye vyeti vyao badala ya kuwanazo kichwani mwao. Jambo hili ndilo linalonitesa moyo wangu jinsi ya kulitatua kwenye akili za watu.

Mfano mwingine: Kama hiyo haitoshi nilipomaliza chuo nilienda sehemu fulani nilikuwa nafanya kazi ya kujitolea ilikuwa ni kwenye halmashauri ya wilaya.  Sikuwa nalipwa mashahara bali nilikuwa napewa posho kidogo kama 3000 kwa siku. Lakini kazi yangu niliyoisomea ilikuwa inanipatia hadi milioni moja kwa mwezi hii ni nje ya posho ya ofisini. Pamoja na kupata pesa hiyo akili yangu iliyokuwa kwenye cheti ilikuwa inalalamika sana si uajiriwe tu. Kwa sababu hiyo nilikuwa naomba usiku na mchana nipate ajira,  na kweli muda haukupita nikapata ajira, kilichonishangaza kwenye ajira mshahara ni mdogo kuliko pesa niliyokuwa naipata kabla sijaajiriwa. Tatizo sio mimi bali ni akili ya kwenye kipande cha karatasi (cheti) ndiyo ilikuwa inafanya kazi badala ya ile iliyoko kichwani.

Kwa mfano huu nimekutana na vijana wengi sana vyeti vyao vinawaendesha vinataka kuajiriwa kwahiyo usiku na mchana hawawezi kufanya mambo mengine kisa hawana ajira ya kudumu. Wanaomba usiku na mchana waingie kwenye system ili wakatumie akili ya cheti badala ya kutumia akili zao zilizomo kichwani. Jambo hili ni moja ya mambo mabaya niliyoyaona duniani.

Athari Za Kuacha Akili Kwenye Cheti
Si kila jambo ni baya.Kuwa na cheti sio vibaya bali kuna faida nyingi zaidi za kuwa na cheti lakini pia kuna hasara nyingi za kuwa na cheti. Sizungumzii kuwa na cheti kama cheti bali nazumgumzia kuacha akili kwenye cheti. Kuacha akili kwenye cheti kunakufanya uwe mtumwa wa cheti chako lakini pia kunakufanya uwe mbumbumbu usiyejua kutumia akili yako nyingi uliyopewa na Mungu wako. Unaweza usinielewe kwa sasa lakini ipo siku utanielewa.

Tunataka kuona matokeo ya elimu yako
Kwa lugha nyingine ni kamba kama umesoma na akili yako unayokichwani hujaiacha kwenye cheti tunategemea kuona matokeo ya elimu yako uliyosoma,  kwa sababu ni lazima tutakuona ukifanya bidii kubuni, kufundisha, kuandika na kufanya kila jitihada kwa ajili yako na kwa ajili ya Taifa lako. Ikiwa hujishughulishi kutengeneza matokeo makubwa yanaoonekana ni dhahiri shayiri kwamba akili zako umeziacha kwenye kipande cha karatasi. Ikiwa unasumbuka na  kuhuzunika eti uajiriwe na hakuna kitu kipya kingine unachokifanya nje ya kuajiriwa niyo ni dalili moja wapo kwamba akili zako ziko kwenye kipande karatasi.

Wazee wetu wa zamani hawakuishi kwa vyeti bali akili zao zilikuwa kichwani mwao, hivi sasa tunashuhudia mambo makubwa waliyoyafanya. Usingeziacha akili zako kwenye cheti ukabaki nazo kichwani ungefanya mambo makubwa sana kwa sababu akili yako ni nyingi mno hujaitumia ipasavyo,  unatumia akili finyu ya kwenye kipande cha katatasi ndiyo maana maisha yako bado hayana mwelekeo sahihi.

Mwisho nakuambia tumia akili iliyoko kichwani mwako, kwa mbali sana unaweza kuchanganya na akili iliyoko kwenye cheti chako kusonga mbele.Kufanikiwa ni maamuzi yako na  inategemea unatumia akili ipi ya kwenye kipande cha karatasi au akili ya kichwani mwako. Amua sasa.

0 comments :

Post a Comment