Ndugu, nakusalimu;
Moja ya changamoto kubwa kabisa kwa watu wengi, ni kupata wazo zuri la biashara. Najua hata wewe ndugu unayesoma makala hili unakubaliana na mimi kwamba kupata wazo zuri la biashara ni mtihani. Unaweza kuwa umejaribu kuulizia watu wengi wakuambie biashara nzuri ya kufanya ni ipi! Najua utakuwa umepata majibu mbalimbali kulingana na uzoefu wa kila mmoja uliye mwuliza.
Ukitazama Neno Biashara Kwa Namna Hii Utaelewa Haraka
Neno biashara ni msamiati wa Kiswahili ambao siku hizi huleta maana zaidi ya moja. Maana ya kawaida, in shughuli yoyote inayohusiana na ubadilishaji na usambazaji na uuzaji wa bidhaa au huduma.
Ubadilishaji huo, katika zama hizi una maana pia ya mapatano ya ubadilishaji huo hata kama bidhaa hizo hazionekani halisi wakati wa mapatano hayo. Hivyo inaweza kufanyika kwa simu, barua pepe, mtandao, barua za kawaida, hata na ana kwa ana. Inawezekana makubaliano hayo au ubadilishaji huo usihusishe ushikaji wa pesa taslimu mkononi. Unaweza kusema kwa maneno mengine kuwa biashara ni uzalishaji na usambazaji wa bidhaa au huduma.
Kwanini Tufanye Biashara?
Chimbuko la biashara ni upungufu wa bidhaa au huduma katika jamii na kutoenea zote, mahali pote kwa wakati zinapohitajiwa. Kama nilivyosema hapo awali, biashara inaweza ikawa kwa mfumo wa huduma mfano shule, zahanati nk. Pia biashara inaweza kuwa katika mfumo wa maneno mfano ushauri (consultancy), na wakati mwingine biashara inaweza kuwa katika mfumo wa dhamana mtu anaweka hati ya mali aliyonayo halafu anapata mahitaji au bidhaa anayohitaji kwa makubaliano ya muda na riba. Kuna namna nyingi za ufanyaji biashara lakini lengo kubwa la biashara ni kusambaza huduma au bidhaa kwenye jamii ili kukidhi mahitaji yanayohitajika.
Biashara Haijaanza Leo Ilikuwepo Tangu Zamani Za Kale.
Historia inatuambia kuwa biashara ilikuwepo tangu zamani sana. Hata kabla pesa hazijagunduliwa biashara ilikuwepo, kipindi hicho biashara iliyokuwepo ilikuwa ni ya kubadilishana bidhaa. Wewe una shaba unabadilishana na mtu mwenye shanga. Au wewe una ng’ombe unabadilishana na mtu mwenye mahindi au mtama nk. Mfumo huu umeendelea kwa karne nyingi hadi pesa zilipogunduliwa zikachukua nafasi yake kama tunavyoona hivi leo. Watu wengi wanaoingia kwenye biashara wanafanikiwa sana kiuchumi hasa pale wanapojitahidi kubuni mbinu nzuri za haraka za kufikisha mahitaji kwenye jamii. Matajiri wakubwa toka enzi za zamani hata hivi leo wameupata utajiri wao kwenye biashara.
Kizazi Kilichoharibu Mawazo Ya Biashara Kwa Watu Wengi Hadi Hivi Leo.
Kipindi cha mapinduzi ya viwanda miaka ya 1700 yalikuja na sera mpya ya ajira. Sera hii mpya ya ajira ilipata nguvu sana kipindi hicho na watu wengi walipata ajira hasa katika nchi za Ulaya na Marekani. Mtu aliyeajiriwa alionekana ni bora kuliko mtu asiye na ajira. Watu wengi walilazimika kusoma ili wapate ajira kwenye taasisi na makampuni ya viwanda. Utaraibu huu wa ajira ulikuwepo hata kabla ya miaka ya 1700 lakini ulipata nguvu kubwa kwenye mapinduzi ya viwanda.
Mawazo haya ya kuajiriwa yamepandikizwa akilini mwetu hivyo imekuwa kila mtu anataka kuajiriwa kwanza badala ya biashara kwanza. Kutokana na mawazo haya, watu wengi sana wamebaki masikini kwa sababu ya kisingizio cha kukosa ajira huku wakisahau kuwa, matajiri wengi hawajaajiriwa bali wameupata utajiri wao kwa njia ya biashara. Kwa sababu ya mawazo ya kuajiriwa watu wengi wamebaki kuwa watumwa wa wenye pesa ambao wengi wao, zaidi ya asilimia 80% ni wafanya biashara.
Mawazo ya kuajiriwa yameleta fikira mgando kuhusu biashara na kwa sababu ya fikira mgando akilini mwa watu kuhusu biashara, kupata wazo la biashara imekuwa shughuli ngumu sana kwa sababu tunefundishwa kuona ajira badala ya kuona biashara. Kwa mantiki hiyo, ikiwa hatuta badili fikira zetu na kuanza kuona biashara kama njia ya kwanza ya kututoa kwenye umasikini, ni dhahiri kwamba kufanikiwa kwetu itakuwa vigumu sana na hivyo kuendelea kubaki watu masikini na wategemezi wa watu wenye pesa ambao ni matajiri. Tusikubali.
Anza Kutazama Kwa Namna Hii Unapotaka Kufanikiwa Kwa Njia Ya Biashara.
Nina rafiki yangu mmoja yeye amemaliza Chuo cha Ardhi Morogoro miaka miwili iliyopita akiwa na kozi ya Upimaji Ardhi (Land Survey). Tofauti na vijana wengi wanaomaliza vyuo, yeye hafikirii kuajiriwa hata siku moja anasema akiajiriwa, ajira itampunguzia kasi yake ya kuufikia utajiri. Kweli mpaka sasa yupo mtaani anapambana kwa kila namna akitumia taaluma yake kupata mtaji na kufanya shughuli nyingine za maendeleo. Ana miaka miwili tu tangu amalize chuo lakini mpaka sasa anajenga nyumba yake kubwa na nzuri pia anamiliki gari nzuri.
Nimekueleza habari hii kwa lengo la kukufanya uanze kufikri kwa namna ya kuitazama biashara kama mkombozi wako wa maisha na hatimaye kufikia mafanikio yako. Najua unaweza ukaanza kuniambia kama sina mtaji wa kuanzisha biashara nitafanyaje? Mimi nasema hicho ni kisingizio tu wala sio kweli kwa sababu kuna njia nyingi sana za kupata mtaji tena hutumii pesa kupata mtaji unatumia maneno tu.
Soma makala hii: Anza Kufanya Kazi Hii Moja Sasa Hivi ,Uone Kama HutapataMtaji Wa Milioni Tano Ifikapo Mwezi Disemba Mwaka Huu
Wazo Zuri La Biashara
Robert kiyosaki, anasema; “Dunia imejaa mawazo mazuri ya biashara, tena dunia imejaa bidhaa nyingi mpya na nzuri. Lakini dunia ina watu wachache wanaofanya biashara”. Kutokana na maneno hayo ya Kiyosaki ambaye pia ni mfanya biashara mashuhuri na tajiri huko Marekani, tunapata kujua kuwa usiumize kutafuta wazo zuri la biashara kwa sababu kuna watu wengi sana wana mawazo mazuri ya biashara vichwani mwao lakini hawajaanza kuyatekeleza, au hata kama wameyatekeleza, wameyatekeleza chini ya kiwango. Kwa hiyo tumia fursa hiyo ya watu kutekeleza mawazo yao ya bishara chini ya kiwango, wewe chukua wazo lao halafu likekeleze kwa ubunifu mkubwa tayari utakuwa umefanikiwa kwenye maisha yako.
Fanya Jambo Hili Moja Tu.
Chagua biashara yoyote unayoipenda moyoni mwako usingalie kuna watu wangapi wanaifanya mtaani kwako, halafu pita kwa wanyabiashara wanaoifanya jifunze kutoka kwao angalia mapungufu yao, wewe anzisha hiyo biashara halafu boresha huduma yako. Mfano mzuri ni wa mfanya biashara maarufu Said Salimu Bakhresa. Alikuwa ana mgahawa wake hapo Kariakoo anapika maandazi na chapati na chips miaka ya 1970. Baada ya kupata akili hii aliamua kuiboresha kazi yake kuzidi wenzake. Kwa sasa ana viwanda vikubwa vya kutengeneza maandazi, chapati, mikate, vinywaji na mengine mengi. Hajatafuta wazo jipya bali kafanya yale yale ambayo wengine wanafanya lakini kaboresha kuliko wengine, hivi sasa ni tajiri wa pili Tanzania nyuma ya Mohamed Dewji.
Pia kuna rafiki yangu mmoja alikuwa anamsimulia jamaa yake jinsi alivyofanikiwa huko Mbeya. Anasema yule jamaa yake alianzisha duka la vyombo ya umeme kama vile luninga, saboofer nakadhalika, sasa ili kuvutia wateja wengi alianzisha wazo jipya la kuwakopesha wateja wake kwa makubaliano maalumu. Anasema, alipata wateja wengi sana alianza na milioni nne kwenye duka hilo hivi sasa anazaidi ya milioni miamoja ndani ya miaka miwili tu.
Chukua Hatua Sasa.
Kama unataka kuwa tajiri, anza kufanya biashara. Kama unataka kubaki kuwa masikini jinsi ulivyo, ng’ang’ana na ajira. Ajira inakufikisha ng’ambo ya kwanza ya mto, unatakiwa uvuke ng’ambo ya pili ya mto ambako ndiko kwenye utajiri na mafanikio makubwa. Kitakachokuvusha mtoni kwenda ng’ambo nyingine ya mto ni biashara. Kama hujapata ajira hilo sio tatizo; kinachotakiwa jifunze kutafuta mtaji bila kutumia gharama yoyote kama nilivyoelezea kwenye makala hii.
Kama wewe bado hujajiunga na mtandao huu, JIUNGEsasa ili uweze kutumiwa makala zetu punde zinapotoka. Tumia email yako kujiunga. Bonyeza neno hili JIUNGE ili ukasome faida nyingine utakazozipata kwa kujiunga na mtandao huu.
Najua unaweza ukaanza kuniambia kama sina mtaji wa kuanzisha biashara nitafanyaje? Mimi nasema hicho ni kisingizio tu wala sio kweli kwa sababu kuna njia nyingi sana za kupata mtaji tena hutumii pesa kupata mtaji unatumia MANENO tu.
0 comments :
Post a Comment